Kilimo cha dengu
Posted in :
Kilimo endelevu cha dengu
Dengu ni zao la jamii ya mikunde linalotoa chakula chenye protini, kusaidia rutuba ya udongo na kufungua fursa za soko la ndani na kimataifa.
Chakula, kipato na udongo wenye afya
Dengu ni chanzo cha protini, nyuzinyuzi, madini na vitamini B. Kwa kuwa ni jamii ya mikunde, husaidia kuongeza rutuba ya udongo; na kwa ubora wa mazao, yana nafasi nzuri katika soko la kimataifa.
Chagua eneo linalofaa
Eneo sahihi, udongo bora na maandalizi ya mapema huweka msingi wa mavuno yenye ubora.
Hali zinazofaa kwa dengu
Chagua eneo lenye udongo mfinyanzi mwepesi hadi wa kichanga, rutuba ya kutosha na usiotuamisha maji.
Maandalizi na upandaji
Fanya uchunguzi wa udongo na andaa shamba mapema, kabla ya msimu kuanza.
Andaa kwa wakati
Andaa shamba mwezi mmoja kabla ya msimu. Lima na kusawazisha kwa wakati, weka matandazo au mabaki ya mazao, na tumia mifereji kwenye maeneo yenye maji mengi.
Tumia mbegu zilizoidhinishwa
Chagua mbegu bora zilizothibitishwa na TOSCI na zinazolingana na msimu, eneo na mahitaji ya soko. Usichanganye aina tofauti shamba moja.
Panda kwa mpangilio
Tumia kilo 20-30 za mbegu kwa ekari. Panda kwenye udongo wenye unyevunyevu kwa nafasi ya sentimita 30 kati ya mistari na 10 kati ya mimea; punje 1-2 kwa shimo, kina cha sentimita 5-8.
Vuna na kausha kwa ubora
Usimamizi mzuri baada ya mavuno hupunguza upotevu wa zao na kuimarisha thamani yake sokoni.
Tambua ukomavu
Vuna baada ya siku 90-115, kulingana na aina ya mbegu. Dalili ni maganda kubadilika rangi kuwa njano, mmea kukauka na mbegu kuwa ngumu. Vuna unyevunyevu ukiwa chini ya 14%.
Kausha na panga
Epuka kugusanisha mavuno na udongo. Pura kwa mashine au fimbo bila kuharibu punje; kausha kwenye turubai safi siku 2-3 hadi unyevunyevu ufikie 12%, kisha ondoa uchafu na punje zilizoharibika.
Uhifadhi na ufuatiliaji wa dengu
Tumia vifungashio safi visivyopitisha hewa, hifadhi sehemu safi, kavu na yenye mzunguko wa hewa, na weka mizigo juu ya chaga ili kuepuka unyevu. Andika kumbukumbu za shamba, mbegu, tarehe za kupanda/kuvuna na matumizi ya pembejeo ili bidhaa ifuatiliwe kutoka shamba hadi sokoni.

